Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akizungumza Dar es Salaam jana
kuwataka mawaziri walioteuliwa kuendelea na nyadhifa zao kubadilika ili
kuleta imani kwa wananchi. Picha na Fidelis Felix
Dar es Salaam. Uamuzi
wa Rais Jakaya Kikwete kuwaacha katika Baraza la Mawaziri, mawaziri
wote waliotajwa na CCM kuwa wameshindwa kutekeleza majukumu yao
umekichanganya chama hicho, baada ya jana kusema kuwa hakitasita
kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri hao na wengine, iwapo watashindwa
kurekebisha upungufu wa kiutendaji unaozikabili wizara zao.
Chama
hicho kilitoa ufafanuzi huo jana ikiwa zimepita siku tano tangu Rais
Kikwete alipofanya mabadiliko katika baraza hilo na kuwaacha mawaziri
saba waliohojiwa na CCM wakidaiwa ni ‘mzigo’, baada ya utendaji wao wa
kazi kulalamikiwa na wananchi pamoja na wabunge.
Desemba
14 mwaka jana CCM kupitia kikao chake cha Kamati Kuu iliwahoji mawaziri
hao, kisha ikamtupia mpira Rais Kikwete kuamua hatima yao, huku
kikifafanua kuwa “kilimshauri mambo matatu; ama kuwafukuza, kuwahamisha
wizara au kuwahimiza wafanye kazi.”
Uamuzi
huo ulikuja baada ya chama hicho kufanya ziara ya siku 26 iliyokuwa
ikiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, mwishoni
mwa mwaka jana katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe na kukumbana na
malalamiko ya wananchi kuhusu utendaji kazi mbovu wa wizara
zinazosimamiwa na mawaziri hao.
Mawaziri
walihojiwa na CCM na wamebakizwa katika Baraza la Mawaziri ni Dk
Shukuru Kawambwa (Elimu), Christopher Chiza (Kilimo), Saada Mkuya
(Fedha). Mkuya alihojiwa kwa niaba ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk
William Mgimwa ambaye kwa sasa ni marehemu). Wengine ni Dk Abdallah
Kigoda (Viwanda), Dk Mathayo David (Mifugo na Uvuvi), Celina Kombani
(Utumishi wa Umma) na Hawa Ghasia (Tamisemi).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema;
“CCM
hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri na watendaji wengine
watakaoshindwa kurekebisha upungufu unaopigiwa kelele. Kushindwa kwao
kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hivyo
chama hakiwezi kuvumilia usaliti huo.”
Alisema
CCM kuendelea kuwafumbia macho watu wasiopenda kuwajibika ni sawa na
kujinyonga chenyewe, kusisitiza kuwa chama kitaendelea na utaratibu wa
kuwahoji watendaji wa Serikali na wasiotaka kuhojiwa wajiondoe
serikalini au watafute kazi nyingine za kufanya. “Wanalipwa mshahara kwa
kodi za Watanzania lazima wakubali kuhojiwa, CCM katika hili tutakuwa
wakali zaidi. Tunaungana na wabunge wa CCM na wananchi kuhusu maoni ya
utendaji kazi wa mawaziri hao, malalamiko yao ndiyo yalizaa neno
mawaziri ‘mzigo” alisema.
Nape alisema chama hicho kitatumia wingi wa wabunge na madiwani wake
kuisimamia Serikali na usimamizi huo kuanzia sasa utaimarishwa zaidi
katika ngazi zote, “Tutaisifu Serikali ikifanya vizuri na tutaikosoa na
kuishutumu ikifanya vibaya.
“Uwajibikaji
wa kweli ndiyo msingi wa mafanikio na maendeleo ya nchi yetu. Tuna
matumaini mawaziri hawatayaangusha matumaini ya wananchi kwa Serikali
yao. Kuteuliwa kwao upya au kuachwa kwenye Baraza la Mawaziri hakufuti
upungufu wao uliotokea siku za nyuma.”
Alisema
ziara za chama hicho pamoja na utaratibu wa kuwahoji watendaji wa
Serikali umekuwa na mafanikio makubwa. Sasa urasimu uliokuwapo awali
katika ununuzi wa pamba, korosho, msongamano wa magari katika mpaka wa
Tanzania na Zambia (Tunduma) na upatikanaji wa mbolea umemalizika.
“Tunaongeza ukali maana muda wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama ni
mdogo, tukicheka na wasiopenda kuwajibika wananchi watatuadhibu.
Hatuko tayari kuadhibiwa kwani tumetoa ahadi kwa Watanzania ni lazima
tuzitekeleze,” alisema Nape.
Huku
akiwataka Watanzania wawape muda mawaziri hao, Nape alisisitiza: “Kama
mambo yasipoenda wananchi waseme na CCM itaungana nao kupiga kelele na
kuhakikisha hatua zinachukuliwa. Ndiyo maana hata wakuu wa mikoa na
wilaya nao wanahojiwa na kutoa ufafanuzi katika masuala mbalimbali.”
Alipoulizwa
kama CCM itaendelea kuwavumilia Dk Kawambwa na Chiza, Nape alisema,
“Wamerudishwa, ila tunatumaini upungufu wameuona, wakishindwa CCM
haitakaa kimya. Ila wananchi wanatakiwa kutambua kuwa kumfukuza waziri
siyo suluhisho.”
Akitoa
mfano, Nape alisema CCM haiwezi kuendelea kuvumilia kuona vinachapishwa
vitabu vya shule za msingi na Sekondari vyenye makosa.
“Mabwana
shamba wiki nzima wanavaa suti badala ya kwenda shambani. Angalia bosi
wao anafanyaje (Chiza). Haiwezekani kwa muda wa miaka minne na nusu
Waziri Chiza hajakwenda kutembelea ghala la taifa la chakula lililopo
mkoani Ruvuma, nasema hivi, ukitaka usinyooshewe kidole kaa nyumbani
kwako.”
Vilevile
alizungumzia jinsi mawaziri wanavyofanya sherehe baada ya kuteuliwa,
“Watu wanadhani kuteuliwa ni ulaji, vijana wa nchi hii wabebe vita hii.
Hivi sasa tukihesabu safari za mawaziri kwenda nje ya nchi na
kuwatembelea wananchi, zipi zitakuwa nyingi?” alihoji.
Kuhusu
madeni ya walimu, alieleza kushangaa kwa nini yanaongezeka kila mwaka
na kuhoji iweje Serikali imefikia hatua ya kuwakopa wananchi badala la
wananchi kuikopa Serikali.” Nape aliponda utaratibu wa watendaji wa
Serikali kufanya vikao kila siku na kushindwa kuwahudumia wananchi, huku
akisisitiza kuwa azimio la Sekretarieti ya CCM ni kuhakikisha kuwa
chama hicho kinakuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao na
kuwasemea wanyonge.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment