Profesa Ibrahim Lipumba, amelishushia
tuhuma nzito Baraza la Mawaziri, baada ya
kudai baadhi ya mawaziri walioteuliwa hawana
elimu ya kutosha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema
mmoja wa mawaziri hao ni Waziri wa Fedha,
Saada Mkuya.
Alisema chama chake, kina wasiwasi na elimu
ya Waziri Mkuya, kutokana na wasifu wake
kutoonyesha vyuo alivyosoma wakati wa
kupata shahada ya kwanza na ya pili katika
masuala ya biashara.
Alisema katika tovuti ya Bunge, wasifu wa
waziri huyo umeonyesha sehemu aliyosoma
elimu ya sekondari na kuhitimu kidato cha
sita.
Alisema katika tovuti hiyo, haionyeshi chuo
alichosoma shahada ya kwanza ya biashara,
ingawa inaonyesha masomo aliyochukua
jambo ambalo linatia mashaka uhalali wake
kuongoza wizara hiyo nyeti.
“Ukiingia kwenye tovuti ya Bunge, utaona
wasifu wake kuanzia elimu ya msingi hadi
kidato cha sita na shule alizosoma, lakini
kuanzia elimu ya shahada imeonyesha
masomo aliyochukua na kupata shahada ya
kwanza ya biashara, haionyeshi vyuo, jambo
ambalo linatia mashaka,” alisema Lipumba.
Alisema nafasi aliyopewa inahitaji kiongozi
mwenye upeo wa hali ya juu, kuweza
kupambanua mambo yanayohusu uchumi wa
nchi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za
kifedha za ndani na nje ya nchi.
“Napata wasiwasi kama Rais Jakaya Kikwete,
aliangalia wasifu wa waziri wake kwa sababu
asingeweza kumchagua kushika nafasi kubwa
kama hii, wakati vyeti vyake vina mashaka,”
aliongeza.
Alisema kitendo cha kumuweka mtu mwenye
vyeti vya mashaka, kunaweza kusababisha
nchi kuyumba kiuchumi, kuongezeka kwa deni
la taifa, kwa sababu uamuzi wake unatokana
na ufahamu wake.
Alisema kutokana na hali hiyo, uamuzi wa
Serikali wa kuwaondoa mawaziri mizigo
hautafanikiwa kwa sababu waziri huyo
anaweza kuongeza mzigo mwingine kwa nchi.
“Mawaziri mizigo, wanaisababishia Serikali
kuwa na viongozi mizigo, hivyo basi
tunapaswa kuwa makini kwa kupinga
kuongozwa na viongozi mizigo, kwa sababu
wanaweza kutuletea matatizo,” alibainisha.
Akitolea mfano katika kipindi ambacho Waziri
wa Fedha anapaswa kuwa makini na matumizi
ya fedha za Serikali, ni pamoja na kuwepo kwa
mchakato wa uboreshaji wa daftari la wapiga
kura, mchakato wa Bunge maalumu la Katiba,
vitambulisho vya uraia na mambo mengine
ambayo kwa kiasi kikubwa yanahitaji fedha.
Alisema kutokana na hali hiyo, waziri huyo
anapaswa kusimamia matumizi ya fedha katika
shughuli mbalimbali zikiwemo za halmashauri
na safari za Rais, ambapo katika kipindi hiki
cha robo mwaka, safari zake za nje zimemaliza
bajeti yake ya mwaka mzima.
Alisema kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete
alipaswa kumchagua mtu makini mwenye sifa
stahiki kukalia nafasi hiyo, ili aweze kutimiza
majukumu yake kwa kufuata taratibu za
kisheria.
Alisema chama hicho hakina mashaka na
uteuzi wake, lakini wana mashaka na chuo
alichosoma na kupata shahada ya kwanza na
ya pili.
WAZIRI AJIBU
Akizungumza na MTANZANIA Jumatatu kuhusu
madai hayo, Waziri Mkuya alisema elimu yake
wala haina mashaka, kwani alisoma kidato cha
tano na sita katika Shule ya Sekondari
Lumumba mjini Zanzibar.
Baada ya hapo, alijiunga na masomo ya
diploma ya Biashara katika Chuo cha Stamford
cha Malaysia, ambapo pia alichukua diploma
nyingine ya biashara nchini Uingereza.
Alisema mbali na masomo hayo, pia amesoma
shahada ya pili ya biashara katika Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania (OUT) na kuhitimu mwaka
2009.
“Nimehitimu Shahada ya Uzamili ya Utawala
na Biashara (MBA) ya Chuo Kikuu cha WATT
kilichopo Edinburgh, Scotland.
“Kwa sasa nachukua Shahada ya Uzamivu
(PhD) ya Utawala wa Biashara Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania, tawi la Dar es Salaam,”
alisema Mkuya.
>>Mtanzania
0 comments:
Post a Comment